Drop Down Menu
FOR VISITORS
Tourism
Work in Zanzibar
Investment
Business
Study in Zanzibar
Immigration

FOR CITIZEN
Travel Documents
Zanzibar ID
National ID
Social Security
Driving Licence
Health System
E-Government
Zanzibar Port
Municipality

Quick Links
Ikulu Zanzibar
Tanzania
Baraza la Wawakilishi
Bunge Tanzania
Zanzibar Electoral Commission
National Electoral Commission

Zanzibar
Zanzibar
Government News Highlights
Hotuba ya Dk Shein wakati wa kulivunja Baraza la nane la Wawakilishi 26/06/2015
HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, WAKATI WA KULIVUNJA BARAZA LA NANE LA WAWAKILISHI, TAREHE 26 JUNI, 2015 Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Waheshimiwa Wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Waheshimiwa Mabalozi wadogo mlioko Zanzibar, Wawakilishi wa Mashirika mbali mbali ya Kimataifa, Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa, Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Assalam Aleikum UTANGULIZI: Mheshimiwa Spika, Awali ya yote, naanza hotuba yangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu; Mwingi wa Rehema na Utukufu kwa kutujaalia afya njema na uhai tukaweza kukutana katika hadhara hii muhimu. Namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kila la kheri katika utekelezaji wa wajibu wetu huu wa kikatiba. Kadhalika, nawapa pole wale wote walioathirika na maafa ya kipindi cha mvua kubwa za hivi karibuni zilizopelekea watu watatu kupoteza maisha na wengine kupoteza mali na uharibifu mkubwa wa nyumba na mazingira. Aidha, tunawashukuru wale wote walioungana na Serikali katika kutoa misaada mbali mbali ya kuwafariji ndugu zetu waliofikwa na maafa hayo. Tunawaomba ndugu zetu hao walioathirika waendelee kuwa na nyoyo za subira na Mwenyezi Mungu awape uwezo wa kukabiliana na mitihani iliyowasibu. Mheshimiwa Spika, Napenda kutoa shukrani za dhati kwako na Baraza lako tukufu kwa kunipa nafasi hii ya kuja kulihutubia Baraza hili la Nane kabla ya kulivunja. Kwa hivyo, kikao hiki cha leo kimeitishwa kwa ajili ya kutekeleza matakwa ya Kikatiba kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa katika Kifungu cha 91(2) (a) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Kadhalika, kikao chetu hiki ni utekelezaji wa Kifungu cha 92(1) cha Katiba ya Zanzibar kuhusiana na uhai wa Baraza la Wawakilishi kuwa ni kipindi cha miaka mitano tangu ulipoitishwa mkutano wa kwanza na leo tarehe 26 Juni, 2015 ndiyo nalihutubia Baraza la Nane kwa mara ya mwisho kabla ya kulivunja ili kupisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Napenda nitumie fursa hii ili nitoe shukrani zangu za dhati kwako Mheshimiwa Spika kwa uongozi wako bora na kwa kazi kubwa uliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano ya Baraza hili, kwa kusimamia na kwa kuziendesha kazi za Baraza kwa mafanikio makubwa. Hongera sana. Shukrani zangu za dhati ziwaendee Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili kwa kuzitekeleza kazi zao kwa moyo wa kujituma, kwa kushirikiana na kwa uvumilivu mkubwa. Ni imani yangu kwamba wananchi wameridhika na namna mnavyowawakilisha mawazo na maelekezo yao katika Baraza hili. Licha ya kuwa na wajumbe wapya wengi katika Baraza hili na upya wa mfumo wa kisiasa tulionao na muundo mpya wa Serikali, mmeweza kuifanya kazi yenu kwa ufanisi mkubwa. Mheshimiwa Spika, Nachukua fursa hii, mimi mwenyewe na kwa niaba ya Serikali kutoa mkono wa pole na rambi rambi kwako, wajumbe wa Baraza lako, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Magomeni na Watanzania wote kwa kifo cha kiongozi mwenzetu Marehemu Salmin Awadh Salmin; aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni na Mnadhimu wa CCM hapa Barazani. Hekima, busara na mchango wake katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kuliendeleza Taifa letu, hautasahaulika na utaendelea kuthaminiwa. Namuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi - Amin. Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza hili la Nane tarehe 11 Novemba, 2010, nilieleza mwelekeo wa mipango ya Serikali nitakayoiunda baada ya wananchi wa Zanzibar kunichagua kwa kura nyingi, kupitia Chama changu cha Mapinduzi, kuwa Rais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 31 Oktoba, 2010. Kadhalika, katika hotuba yangu hiyo, nilisema kuwa tunaianza Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tukiwa na dhima ya msingi ya kuwatumikia wananchi waliotuchagua kwa kipindi cha miaka mitano. Matumaini ya wananchi kwa Serikali yao yalikuwa ni kuyaendeleza mafanikio yote yaliyoletwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa awamu zote zilizotangulia na kutekeleza sera na mipango itakayowezesha kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii. Ili kuyafikia malengo hayo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba inaongozwa kwa kuzingatia mipango mikuu ya kitaifa ambayo ni Dira ya Maendeleo ya 2020, Malengo ya Milenia, MKUZA na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 hadi 2015. Sambamba na hayo, utekelezaji wa ahadi nilizozitoa katika kampeni ya uchaguzi ya mwaka 2010 ilikuwa ni miongoni mwa vipaumbele muhimu katika utendaji wa serikali niliyoiunda. Mheshimiwa Spika, Leo nitaelezea kwa muhtasari mafanikio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika nyanja zote za maendeleo, kisiasa, kiuchumi na ustawi wa jamii. Ni dhahiri kuwa mafanikio hayo yanatokana na mchango wenu katika kutekeleza wajibu, kufuatana na Mipango mikuu ya kitaifa niliyoeleza hapo mwanzo na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015. Ilani hiyo ni mkataba baina ya wananchi na Serikali yetu. Ni jambo la kufurahisha kwamba hadi leo hii, Ilani hiyo imeshatekelezwa kwa kiwango kinachokadiriwa kufikia asilimia 90. Natoa pongezi kwa wale wote walioshiriki katika utekelezaji wa Ilani hii. Siri kubwa ya mafanikio yetu ni kuwa sisi tuliingia katika muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa tukiwa tayari tunayo Katiba iliyoandaliwa kwa ajili ya Muundo huo. Lakini zaidi ya hayo, tulidhamiria kwa dhati kuitekeleza azma na shabaha ya muundo huo. Tulijenga heshima na mapenzi baina yetu. Tulijenga misingi ya kuvumiliana. Kwa kufanikisha uendeshaji wa serikali, nilipanga Wizara na kuteua Mawaziri kwa uwiano wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar. MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MIPANGO YA SERIKALI: HALI YA UCHUMI: Mheshimiwa Spika, Katika kipindi hiki kuanzia mwaka 2010 – 2014, Pato la Taifa kwa bei za miaka hio limekua kutoka TZS bilioni 1,050.8 hadi kufikia TZS bilioni 2,133.5. Kwa bei za kudumu, Pato la Taifa limekua kutoka TZS bilioni 848.2 hadi kufikia TZS bilioni 1,115.4 sawa na ukuaji wa asilimia 31.5 kwa kipindi hicho. Uchumi wetu umekua kutoka asilimia 4.3 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.0 mwaka 2014 sawa na ongezeko la asilimia 2.7. Pato la Taifa kwa mwananchi mmoja, kwa bei za miaka 2010 – 2014, limekua kutoka TZS 856,000 ($613) mwaka 2010 hadi kufikia TZS 1,552,000 ($939) kwa mwaka 2014. Katika kipindi cha mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015, mapato ya ndani yameongezeka kutoka TZS bilioni 181.4 hadi kufikia TZS bilioni 360.4, sawa na ukuaji wa asilimia 98.7 kwa kipindi hicho au wastani wa asilimia 19.7 kwa kila mwaka. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa mfumko wa bei, tunaendelea kuwa na mfumko wa bei ulio katika tarakimu moja. Katika mwaka 2010, mfumko wa bei ulikuwa wa wastani wa asilimia 6.1 na umeshuka kufikia wastani wa asilimia 5.6 kwa mwaka 2014. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016, Bajeti yetu itaendelea kuzingatia malengo makuu ya Serikali. Malengo hayo ni kujenga jamii: (i) Iliyoelimika kwa elimu bora na inayotoa wataalamu wenye hadhi ya kimataifa; (ii) Yenye siha, (ii) Iliyoimarika kiuchumi; na (iv) Inayojali Umoja wa Kitaifa na kufuata misingi ya Utawala Bora. Mambo haya ndio yanayojenga falsafa iliyomo katika Dira ya Maendeleo ya 2020 ambayo inatekelezwa kwa sasa kupitia MKUZA II na Mpango wake wa utekelezaji. Utendaji wa sekta zote umejielekeza katika kufikiwa kwa malengo hayo makuu. Mheshimiwa Spika, Katika kuinua uchumi wetu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika kila wizara kwa lengo la kutilia mkazo umuhimu wa utafiti katika maendeleo yetu. Serikali, kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (COSTECH) imeendeleza tafiti katika taasisi mbali mbali ikiwemo Kilimo, Elimu, Uvuvi na Nyanja nyenginezo. MATOKEO KWA USTAWI: (RESULTS FOR PROSPERITY - R4P) Mheshimiwa Spika, Katika kutafuta mbinu bora za kutekeleza mipango yetu, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwakutanisha wataalamu wa sekta mbali mbali kwa mfumo uliopewa jina la Mpango wa Maabara kwa ajili ya kujadili, kupanga na kupitisha maazimio ya utelekezaji wa mipango mbali mbali ya maendeleo. Utaratibu huu, hapa petu, tumeufuata na tumeupa jina la Matokeo kwa Ustawi (Results for Prosperity - R4P) ambao umeonesha kuwa na mafanikio makubwa kwa nchi zilizouanzisha na kuufuata. Hivi karibuni Serikali imeanza kutekeleza programu mbali mbali zinazotayarishwa katika Mpango wa Matokeo kwa Ustawi. Programu zilizoanza kutekelezwa ni pamoja na Programu Mjumuisho ya Kuendeleza Utalii, Programu ya Kuimarisha Mazingira ya Biashara na Mkakati wa Utafutaji Rasilimali Fedha. Kwa sasa mchakato unaendelea wa matayarisho kwa ajili ya sekta afya na elimu ambazo tunatarajia zitaanza katika mwaka huu. MIRADI YA MASHIRIKIANO BAINA SEKTA YA UMMA NA SEKTA BINAFSI: Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miaka mitano, tumefanya jitihada kubwa za kuiimarisha na kuishirikisha Sekta binafsi katika mipango yetu ya maendeleo. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeanzisha kitengo cha “PPP” katika Tume ya Mipango kwa ajili ya kushughulikia miradi itakayoanzishwa kwa mfumo huo. Serikali imejiandaa kuanzisha Idara kamili ya “PPP” ambayo itahusika na utekelezaji na usimamizi wa shughuli zote za miradi ya mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. UWEKEZAJI VITEGA UCHUMI: Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, kupitia Mamlaka ya Vitega Uchumi (ZIPA) ilifanya kazi nzuri katika kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani kuja kuwekeza katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii. Kwa Kipindi cha miaka mitano (2010 – 2015), tumeweza kusajili miradi 187 yenye thamani ya TZS milioni 38,560.50, sawa na USD 1,881,00 milioni ambayo inakadiriwa kuwapatia ajira watu 9,192. Wawekezaji kutoka Uturuki, China, Italia, Ujerumani na India wameonesha dhamira ya dhati ya kutuunga mkono na nimetumia fursa niliyoipata kuwakaribisha waje kuwekeza, wakati nilipotembelea nchi zao, vile vile wawekezaji wa ndani nao wamehamasika katika uwekezaji kwenye nyanja mbali mbali. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), kuanzia mwaka wa fedha 2014/2015, imeweka mkazo mkubwa katika kukamilisha dhamira ya kuendeleza maeneo huru ya uchumi. Ni dhahiri kwamba mpango huu tangu ulipobuniwa na hatimae kutolewa tangazo la Sheria Namba 5 la mwaka 1993 bado hazijachukuliwa juhudi za kutosha za kutekeleza kwa vitendo uendelezaji wa maeneo hayo. Kwa hakika hivi sasa tumejidhatiti kuitekeleza dhana ya maeneo huru ya uchumi kwa vitendo. Mipango yetu ni kuibadilisha taswira ya eneo la Fumba. Tumepanga kuutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Mji wa Kisasa wa Fumba (Fumba Bay Satellite City Project). Mji huu mpya wa kisasa na wa kibiashara utakuwa na mtaa mkubwa wa biashara (High Street), nyumba za kisasa za kibiashara za kuishi wageni na wenyeji na uwanja wa kuchezea mchezo wa gofu. Vile vile, kutakuwa na hoteli moja kubwa ya nyota tano yenye vyumba 400 na tutajenga eneo la shughuli za biashara ambalo litakuwa na maghala ya kisasa na mfumo wa usafirishaji wa bidhaa wa kisasa. Aidha, katika mji huu kutakuwa na uwanja wa mpira wa kisasa ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua kiasi cha watu 45,000. Pamoja na huduma za kijamii za ulinzi, afya na elimu, mradi huo unakusudia kuanzisha bandari ndogo kwa ajili ya huduma za usafiri wa majini kati ya Zanzibar - Pemba na Zanzibar - Dar es Salaam. Jumla ya hekta 700 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Serikali imeanza mazungumzo na Muwekezaji wa Kampuni mama ya Bakhresa Group juu ya kushirikiana katika uwekezaji wa mradi huu kwa mfumo wa ubia (joint venture company). Mheshimiwa Spika, Vile vile, katika eneo hili tutatekeleza Mradi wa Mtaa wa Viwanda. Jumla ya hekta 100 zimetengwa katika maeneo ya Dimani, Kusini pamoja na Ndambani kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za viwanda vidogo na vya kati. Mazungumzo yanaendelea kati ya Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) na Kampuni ya CPC ya Misri juu ya mfumo na utaratibu na ushirikiano wa uwekezaji wa Miundombinu katika eneo hilo. Kadhalika, Hekta 60 zimetengwa kwa ajili ya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na kukabidhiwa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kwa ajili ya kuandaa maelezo maalum ya mradi wa uwekezaji. Maelezo hayo yakiwa tayari, Mamlaka itashirikiana na Wizara hiyo kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji utakaopangwa. Mheshimiwa Spika, Vile vile, Serikali imebuni mpango wa kutekeleza Mradi wa Uendelezaji wa Mji wa Nyamanzi – Fumba. Mradi huu umetengewa kiasi cha hekta 63 ambazo zitatumika kwa ajili ya nyumba za makaazi na biashara mbali mbali ikiwemo maeneo ya makaazi ya kijamii, majengo ya kuishi, huduma za hoteli na kumbi za mikutano, huduma za masoko na mawasiliano, maofisi na maduka pamoja na maegesho ya magari, vituo vya ferry, maeneo ya burudani afya na michezo. Maeneo ya asili ya vijiji vya eneo hilo vikiwemo Fumba, Bweleo, Dimani na vijiji vyengine vidogo vidogo yataheshimiwa na kuendelezwa kwa mashauriano na wanavijiji wenyewe. Mheshimiwa Spika, Katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, tumeshaanza Mradi wa Maendeleo ya Mji wa Kisasa Kijini – Matemwe. Mradi huu unaendelea kutekelezwa na Kampuni ya “Penny Royal” katika maeneo ya Matemwe Muyuni, ambapo utagharimu jumla ya Dola za Kimarekani milioni 220. Mradi huo unajumuisha ujenzi wa Hoteli ya kimataifa yenye hadhi ya nyota tano. Aidha, mradi huo utahusisha ujenzi wa kiwanja cha kimataifa cha gofu, chenye jumla ya vishimo 18 na ujenzi wa nyumba za makaazi kwa watu wenye kipato cha juu ambazo zitatumia nishati ya nguvu ya upepo. Hivi sasa Kampuni hiyo inaisaidia Serikali katika ujenzi wa barabara yenye urefu wa km 20.2 kutoka Matemwe kupitia Kijini kuelekea maeneo ya mradi hadi Kidoti. Ujenzi wa barabara hio unaendelea vizuri. Mheshimiwa Spika, Katika eneo la Mjini Unguja, katika kipindi hiki, Serikali imepanga kutekeleza Mradi wa Kuendeleza Hoteli ya Bwawani na eneo linaloambatana nalo. Serikali italiendeleza eneo hilo kupitia Muwekezaji wa Kampuni ya “Quality Group” alieshinda zabuni. Kampuni hii inakusudia kuendeleza eneo la Bwawani kwa kujenga Hoteli ya Kisasa ya nyota tano, majengo ya kisasa ya makaazi, majengo ya biashara, mikahawa, soko la Kizanzibari na maegesho ya magari. Jengo la sasa la hoteli ya Bwawani litakarabatiwa kwa ajili ya kupokea wageni mashuhuri. Uendelezaji wa eneo la Bwawani utazingatia ipasavyo athari za Kimazingira na urithi wa kale. SEKTA YA BIASHARA NA VIWANDA: Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi. Usafirishaji wa bidhaa unaendelea kuimarika mwaka hadi mwaka. Katika mwaka 2014 tumeweza kuuza nje bidhaa zenye thamani ya TZS milioni 133,591.7 kutoka bidhaa zenye thamani ya TZS milioni 87,799.6 mwaka 2013, sawa na ongezeko la asilimia 52.14. Usafirishaji huo umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na jitihada zetu za kuimarisha uzalishaji wa zao la karafuu na mwani ambayo usafirishaji wake ulifikia TZS milioni 103,079.2 kutoka TZS milioni 75,392.6 mwaka 2013. Hili ni ongezeko la asilimia 77.8 ya usafirishaji wote kwa mwaka 2014. Licha ya kuwepo kwa urari kwa bidhaa kwa usafirishaji nje, takwimu hizi zinatupa matumaini mazuri juu ya mwenendo na ukuaji wa biashara nchini. Kuhusu biashara baina Zanzibar na Tanzania Bara, jumla ya bidhaa zenye thamani ya TZS milioni 23,268.7 ziliingizwa Zanzibar kutoka Tanzania Bara mwaka 2010 ikilinganisha na bidhaa zenye thamani ya TZS milioni 64,296.4 mwaka 2014. Vile vile, bidhaa zenye thamani ya TZS milioni 2,203.8 zilisafirishwa kwenda Tanzania Bara mwaka 2010 ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS 366,354.2 mwaka 2014. Kwa jumla, katika kipindi hiki cha kwanza cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, urari wa biashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara unaendelea kuwa mzuri kwa upande wa Zanzibar. Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kuwa juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, za kufufua zao la Karafuu zimezaa matunda mazuri. Mpango wa miaka kumi wa kufufua zao hili, tumekuwa tukiutekeleza kwa mafanikio. Katika kipindi cha miaka mitatu ya kwanza ya mpango huo; 2011/12 - 2013/2014, jumla ya tani 11,477 za karafuu zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 130.82 zilisafirishwa na kuuzwa nje ya nchi. Kiwango hicho ni sawa na ongezeko la tani 2,792 ambalo ni sawa na asilimia 32.1 ikilinganishwa na mwaka 2008/09 - 2010/2011. Hadi kufikia tarehe 12 Juni, 2015 jumla ya tani 2, 822 zenye thamani ya TZS bilioni 39.48 zilinunuliwa kutoka kwa wakulima. Mheshimiwa Spika, Serikali imetimiza ahadi niliyoitoa mwaka 2011 ya kuwalipa wakulima wa zao la Karafuu asilimia 80 ya bei ya karafuu ya Soko la Dunia. Karafuu za Daraja la Kwanza zinanunuliwa kwa bei ya TZS 14,000 kwa kilo badala ya TZS 5,000 kwa kilo, bei iliyokuwepo mwaka 2010. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 180. Kadhalika, vituo vipya vya ununuzi na uuzaji wa karafuu vimejengwa Unguja na Pemba, vituo vya zamani vimekarabatiwa na huduma zote muhimu zinapatikana kwenye vituo hivyo. Tumefanikiwa sana katika kupambana na Magendo ya Karafuu na wananchi wanauza Karafuu zao katika Vituo vya ZSTC. Tunawashukuru Wananchi na Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri, walioifanya ya kushirikiana na Serikali katika kupambana na Magendo ya Karafuu. Mheshimiwa Spika, Maamuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ya kulifanyia mageuzi Shirika la ZSTC yamekuwa na manufaa makubwa kwetu. Ni habari njema kwetu sisi viongozi na wananchi kutambua kwamba Shirika limegeuka kutoka kuendeshwa kwa hasara kuwa Shirika lenye kuendesha shughuli zake kwa faida. Hivi sasa Shirika linalipa kodi ya mapato na kulipa faida nyengine Serikalini. Imebainishwa kuwa kwa hesabu zilizokaguliwa katika mwaka wa 2011/2012, 2012/2013 pamoja na makadirio kwa hesabu za 2013/2014 Shirika limelipa jumla ya TZS 1.8 bilioni kama kodi ya mapato na kulipa gawio la TZS milioni 500 kwa mwaka 2013/2014. Nachukua nafasi hii kutoa pongezi kwa Uongozi na Wafanyakazi wa ZSTC kwa mafanikio haya. Mafanikio yaliyopatikana katika kuliimarisha zao la karafuu, kupambana na magendo na kulifanyia mabadiliko Shirika la ZSTC, yametokana na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya 2010/2015 ya kutolibinafsisha zao la karafuu, lakini uandaliwe mpango madhubuti wa maendeleo ya karafuu. Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika kukuza uchumi na kuimarisha Soko la Ajira, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ilipanga na kutekeleza mipango mbali mbali yenye lengo la kukuza sekta ya viwanda. Ongezeko la bidhaa zinazozalishwa viwandani katika kipindi hiki cha miaka mitano linatupa matumaini na ari ya kuendeleza kwa kasi zaidi. Thamani ya bidhaa zilizozalishwa viwandani imeongezeka kutoka TZS bilioni 128 mwaka 2013 hadi kufikia TZS 136 bilioni mwaka 2014. Hili ni sawa na ongezeko la asilimia 5.5. Wawekezaji wamekuwa wakiwekeza katika viwanda vya usafishaji nafaka, usindakaji maziwa, uzalishaji sukari, maji ya kunywa na vinywaji mbali mbali. Aidha, pamekuwa na ongezeko la ukuaji wa viwanda vidogo vidogo vinavyozalishwa na wajasiriamali wanaozalisha sabuni, vifaa vya ujenzi, samani na bidhaa za viungo Unguja na Pemba. Ukuaji huo vile vile umepelekea kuwepo kwa ongezeko la mchango wa sekta hii kwa Pato la Taifa ambapo katika mwaka 2014 ulifikia asilimia 9.9 kutoka asilimia 6.9 mwaka 2013. Taasisi ya Viwango tuliyoianzisha baada ya kupitisha Sheria ya Viwango Namba 1 ya mwaka 2011 imeanza kazi zake katika kuimarisha bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini. Tunaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha sekta ya Viwanda na Biashara ikiwa ni pamoja na kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na Baraza la Biashara la Zanzibar (ZNBC) katika mikutano ya kila mwaka tunayoendelea kuifanya. Natoa shukurani kwa wajumbe wa ZNBC na wale wote wanaoshiriki katika mikutano ya mwaka ya Baraza hili kwa michango na mashirikiano wanayotoa kwa lengo la kukuza sekta zetu muhimu za uchumi hasa Biashara, Viwanda na Utalii. Aidha, natumai kwamba juhudi zetu za kuanzisha Tamasha la Biashara zitakuwa na mchango mkubwa katika kutangaza na kukuza biashara, viwanda na shughuli mbali mbali za ujasiriamali zinazoendeshwa nchini. UTALII: Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miaka mitano, tumefanikiwa sana kuiendeleza sekta ya utalii. Tumeitekeleza kwa mafanikio dhana ya utalii kwa wote niliyoitangaza rasmi tarehe 16 Oktoba, 2011. Serikali imeifanyia marekebisho Sheria ya utalii ya mwaka 2009, na kupelekea kuundwa kwa Sheria mpya Namba 7 ya mwaka 2012 ambayo inakidhi haja na kwenda sambamba na dhana ya utalii kwa wote na kutoa miongozo imara ya kuiendesha sekta hiyo. Takwimu zinaonesha kuwa Idadi ya watalii 132,836 walitembelea Zanzibar katika mwaka 2010; ambapo katika mwaka 2014 watalii wapatao 311,801 waliwasili Zanzibar. Hili ni ongezeko la asilimia 134 katika kipindi cha miaka minne. Katika kuhakikisha usalama wa wananchi na wageni wanaotutembelea, Serikali imeandaa Mradi wa usalama katika maeneo ya Mji wa Unguja. Jumla ya fedha kwa mradi wote kwa kipindi cha miaka mitano ni Dola za Marekani Milioni 28.9. Fedha zilizotengwa kwa matumizi ya mwaka wa kwanza ni TZS bilioni 10. Mradi huu utatupatia vifaa vya CCTV, magari ya zimamoto, boti za doria na mashine ya kukagulia vifaa vya hatari vilivyofichwa katika magari. Vifaa hivyo tayari vimeshaagiziwa na Kampuni ya RAVITALCO ya Romania na ROM SOLUTION iliyosajiliwa Zanzibar. Vile vile, kwa kushirikiana na Kampuni ya Mawasiliano ya ZTE ya China tayari tumeshafunga kamera maalum za usalama (CCTV) katika maeneo ya Mji wa Unguja. Kadhalika, kwa lengo la kuimarisha ulinzi kwa watalii, Serikali imeanzisha Kampuni ya Ulinzi ya JKU, ambayo itatoa huduma kwa sekta binafsi kwenye mahoteli. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi hiki cha miaka mitano, tumeshuhudia ongezeko la wawekezaji katika ujenzi wa hoteli za kisasa zenye hadhi ya juu. Aidha, tumeshuhudia ongezeko la vivutio vya utalii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanja vya mchezo wa gofu ambao unapendwa na watalii. Kumekuwa na ongezeko la idadi ya wageni wanaotoka Mashariki ya Kati na Mashariki ya mbali baada ya kuongeza juhudi za kuitangaza Zanzibar katika maeneo hayo mapya. Chuo cha Maendeleo ya Utalii nacho kimeimarishwa ili kiendelee kutoa rasilimali watu wenye ujuzi, taaluma na stadi zinazohitajika na wawekezaji wanaokuja nchini. MAKUMBUSHO NA MAMBO YA KALE: Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miaka mitano, tumefanya jitihada za pamoja katika kufanya matengenezo ya makumbusho na kuyatunza mapango mbali mbali. Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya Urithi wa Utamaduni itakayotoa muongozo wa matumizi bora ya maeneo ya urithi ili kuimarisha shughuli za utalii. Miongoni mwa maeneo ya historia, mambo ya kale na urithi wa utamaduni tuliyoweza kuyaimarisha ni Mangapwani, Kuumbi Jambiani na Kwa Bi. Khole kwa upande wa Unguja na Chwaka - Tumbe kwa upande wa Pemba. Natoa wito kwa wananchi waendeleze utamaduni wa kuyatembelea maeneo yetu hayo ili kuimarisha utalii wa ndani. SEKTA YA KILIMO: Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua kuwa, kilimo ndio chanzo kikuu cha ajira za wananchi kwa asilimia 70 ya ajira na kinatoa asilimia 27.3 katika Pato la Taifa, niliahidi Serikali itafanya juhudi ya kuiendeleza sekta hii kwa kauli mbiu ya Mapinduzi ya Kilimo. Serikali imefanya jitihada mbali mbali ili kuongeza uzalishaji wa mazao hasa mpunga ili kuwa na uhakika wa chakula na lishe. Serikali imenunua pembejeo mbali mbali za kilimo, imeajiri wataalamu wa ugani na imetekeleza programu niliyoianzisha mwaka 2011 ya kuwapa ruzuku wakulima ya asilimia 75 ya gharama za bei ya mbolea, mbegu, dawa ya magugu na huduma za matrekta. Jitihada hizo za Serikali ziliweza kuzaa matunda kwa kuongezeka kiwango cha uzalishaji. Mavuno ya zao la mpunga kwa jumla yameongezeka kutoka tani 21,014 mwaka 2010 hadi tani 33,655 mwaka 2013. Hili ni sawa na ongezeko la asilimia 60. Katika kipindi hiki Zanzibar imepata mafanikio makubwa ya uzalishaji wa mazao muhimu ya chakula hadi kufikia tani 674,334. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imefanya jitihada za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji maji ili kupunguza tatizo linalotukumba katika kilimo cha kutegemea mvua zisizo za uhakika. Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji wa hekta 2,200 katika mabonde ya Cheju, Kibokwa, Kilombero, Mlemele na Makwararani umeanza kushughulikiwa kwa hatua mbali mbali. Kadhalika, kwa kutambua umuhimu wa utafiti katika kuleta maendeleo ya kilimo, Serikali imefanya jitihada za kukiimarisha kituo cha utafiti wa kilimo Kizimbani kwa kukipandisha hadhi kuwa Taasisi ya Utafiti ya Kizimbani. Taasisi hii imeshirikiana vyema na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (COSTECH) katika shughuli za utafiti. Jumla ya mbegu 43 zimefanyiwa utafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa zao la Mpunga wa Kimataifa (IRRI). Kadhalika, Taasisi hii imefanya tafiti juu ya mbegu za mazao ya mizizi na kutoa mbegu zinazostahamili maradhi na kunawiri katika mazingira yetu. Katika kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za mazao mbali mbali, Serikali imekuwa ikiendeleza majaribio ya mbegu ya mpunga ya NERICA katika vituo vya Mwera na Kizimbani. Hivi sasa wakulima tayari wameshapatiwa mbegu hii kwa ajili ya uzalishaji na kuiendeleza. Tafiti mbali mbali zimeonesha kuwa hii ni mbegu bora kwa mazingira yetu kwa kuwa inastahamili ukame na inastawi hata katika ardhi isiyo ya mabondeni. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya juhudi kubwa katika kuhifadhi misitu na miti yetu ya asili. Zanzibar imejaaliwa kuwa na miti ya aina mbali mbali ya asili ambayo idadi yake imeanza kupotea na hatukuwa na utaratibu bora wa kuitunza. Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali ilifanya jitihada za kuendesha sensa ya miti mwaka 2013 ili kujua idadi ya miti iliyopo. Pamoja na jitihada hizo, Serikali imeongeza juhudi za uhifadhi wa misitu yetu ya asili ikiwa ni pamoja na msitu wa Jozani, Ufufuma, Kiwengwa na Makangale pamoja na kusimamia Mradi wa Hifadhi ya Misitu ya Asili (HIMA) katika maeneo mbali mbali, Unguja na Pemba. Kwa lengo la kuongeza idadi ya miti tuliyonayo, katika kipindi hiki jumla ya miti milioni 5 ya misitu ilioteshwa katika vitalu vya Serikali na miche milioni 8 katika vitalu vya watu binafsi. Jitihada maalum zimefanywa katika kuimarisha kilimo cha karafuu, ambalo ni zao letu kuu la uchumi. Serikali imewahamasisha wakulima wa zao hilo kuyaendeleza mashamba yao na kuwapatia miche bila ya malipo. Hatua hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa mpango wa miaka kumi wa kulifufua zao la karafuu. Katika kipindi cha 2010-2014 jumla ya miche ya mikarafuu milioni 3.7 iligawiwa kwa wakulima katika lengo lilokusudiwa la kutoa miche milioni 3.8. MIFUGO NA UVUVI: Mheshimwa Spika, Katika sekta ya mifugo, Serikali iliweka malengo ya kuleta mapinduzi ya ufugaji ili kuongeza tija na ubora wa mazao yanayotokana na shughuli hiyo. Dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa na ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi na kuku kwa lengo la kuongeza tija na kipato cha wafugaji wetu. Soko la maziwa sasa limekua kutokana na muwekezaji Mzalendo (kufungua kiwanda cha maziwa) Fumba. Serikali vile vile, imeimarisha maabara ya mifugo Maruhubi kwa kuifanyia matengenezo makubwa, kuweka vifaa vya kisasa vya kuhifadhia mbegu bora za ng’ombe na kuendeleza mradi wa upandishaji ng’ombe kwa shindano ili kupata ng’ombe bora. Kadhalika, Serikali iliendesha mradi wa kudhibiti maradhi ya mifugo yasiyo na mipaka ambapo ng’ombe 20,000 walichanjwa kwa kuwakinga na maradhi ya chambavu na kimeta na kuku 80,000 walichanjwa ili kuwakinga na mahepe. Mheshimiwa Spika, Nilianzisha Mapinduzi ya uvuvi kama nilivyotamka katika Hotuba yangu ya tarehe 11 Novemba, 2010, katika Baraza hili. Mwaka 2010 tuliahidi kufanya jitihada za kuziimarisha shughuli za uvuvi kwa kutambua umuhimu wake katika kutoa ajira, kutupatia lishe bora na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa. Nina furaha kuwa Serikali imepata mafanikio katika utekelezaji wa azma hiyo ambapo mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa umefikia asilimia 7.2. Jumla ya tani 148,535 za samaki zenye thamani ya TZS bilioni 527.5 zimevuliwa hadi mwaka 2014. Ni jambo la kutia moyo, kuona kuwa jitihada za Serikali za kushirikiana na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya uvuvi haramu na kuimarisha hifadhi ya mazingira ya bahari zimesaidia sana kuongeza kiwango cha samaki wanaovuliwa. Jumla ya wavuvi wapatao 2,520 wamepatiwa mafunzo ya uvuvi bora yakiwemo ufugaji wa samaki na viumbe wengine wa baharini. Serikali imeandaa mpango wa ujenzi wa kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki katika eneo la Beit - el-Ras na imetoa mafunzo kwa wafugaji wa samaki 69 kuhusu utengenezaji wa chakula, ulishaji, uchimbaji wa mabwawa na utunzaji bora wa samaki. Mheshimiwa Spika, Wakati huo huo, zao la mwani ni miongoni mwa mazao ya baharini na kutupatia fedha za kigeni. Jumla ya tani 51,687 za mwani mkavu zenye thamani ya TZS bilioni 187 zimesafirishwa nje ya nchi katika kipindi hiki. Serikali imewapatia vihori wakulima wa mwani wa Unguja na Pemba kwa ajili ya kubebea mwani. Tunafanya juhudi kuwapa nguvu wakulima wa mwani ili kuhakikisha zao hili linasarifiwa hapa nchini kwa lengo la kukuza uchumi wetu na kuongeza kipato cha wakulima wetu. Aidha, kufuatia safari yangu ya China na Vietnam niliwashajihisha wawekezaji kushiriki katika sekta hiyo. Matumaini yetu ya utekelezaji ni mazuri. Kwa lengo la kuongeza mapato yanayotokana na uvuvi, Serikali imejiwekea lengo la kuanzisha programu ya uvuvi wa bahari kuu. Programu hii inakusudiwa kuwawezesha wavuvi wetu kuvua katika kina kirefu cha maji ili kuongeza kiwango cha samaki wanaovuliwa na kuongeza fursa za ajira, biashara na kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Programu hiyo itaendeshwa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA). Maandalizi ya programu hiyo yamekwishaanza. Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa mpango wa kuendeleza uvuvi wa bahari kuu kwa lengo la kuwawezesha wavuvi na vifaa kuongeza kipato chao. Serikali imefikia makubaliano na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kuimarisha diko na soko la samaki la Malindi ili liwe la kisasa na lenye uwezo wa kuhudumia vyombo vya uvuvi ikiwemo vinavyovua bahari kuu. Utekelezaji wa mradi huo utakaogharimu Dola za Marekani 244,500 na utaanza mwaka huu. Utakapomalizika utawanufaisha wananchi wengi. Kadhalika, Serikali imewakaribisha wawekezaji kwa makubaliano ya kuwashirikisha wavuvi wazalendo. Katika mwaka 2015, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imefikia makubaliano ya awali na Mwekezaji (Hairu Fisheries Management Company) kutoka Sri Lanka ya kuleta vyombo 20 vya urefu wa mita 18 ambavyo vina uwezo wa kuvua katika kina kirefu na kukaa baharini kwa muda mrefu. Aidha, Mwekezaji huyo atajenga Kiwanda cha Boti za Uvuvi za mita 6 na mita 9 ambazo watauziwa wavuvi wetu. Hatua hizo zitaimarisha juhudi za Serikali za kuwawezesha wananchi kuitumia raslimali ya bahari kuu kujiongezea kipato chao. MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa hifadhi ya mazingira katika utekelezaji wa mipango yetu yote ya maendeleo na imechukua jitihada za kukabiliana na uharibifu wake unaosababishwa na wanadamu na ule unaotokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali ni kuandaa Sera mpya ya Mazingira ya mwaka 2013 yenye kutoa muongozo kwa shughuli za uhifadhi wa mazingira nchini na kutayarisha Sheria mpya ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2015. Serikali imezingatia haja ya kufanya tathmini ya athari za mazingira katika miradi ya uwekezaji ambapo jumla ya tathmini 71 za athari za mazingira zimefanywa na wahusika kupewa vyeti. Kadhalika, miradi 221 imefanyiwa ufuatiliaji wa kimazingira na kutolewa ushauri. Vile vile, Serikali imechukua hatua za kukabiliana na athari za tabia nchi. Mheshimiwa Spika, Mnamo mwezi Septemba, mwaka 2014 nilihudhuria mkutano wa nchi ndogo za visiwa zinazoendelea nchini Samoa, kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Tanzania ilipata heshima ya kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa mkutano na nikapewa heshima ya kuhutubia kikao cha ufunguzi uliofanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban ki Moon. Tukio moja wapo muhimu wakati wa mkutano huo ni uzinduzi wa Mpango wa Magharibi ya Bahari ya Hindi wa changamoto za Ukanda wa Pwani na Mabadiliko ya Tabianchi (Western Indian Ocean Coastal Challenge (WIOCC). Visiwa vinavyoshiriki mpango huo ni pamoja na Sychelles, Comoro, Mauritius, Reunion na Zanzibar. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa nchi za visiwa pamoja na Washirika wa Maendeleo wakiwemo Island Partnership (GLISPA). VYAMA VYA USHIRIKA NA SACCOS: Mheshimiwa Spika, Wananchi wamefaidika na taasisi hizo kwa kujipatia ajira na mikopo ya kujiendeleza. Ili kukuza taaluma ya vyama vya ushirika na SACCOS zilizopo, Serikali imeandaa mpango mkuu wa mafunzo wa miaka mitatu (Training Master Plan), pamoja na kuandaa miongozo ya aina 13 ya kufundishia kwa mujibu wa mahitaji ya mafunzo yaliyoibuliwa. KAZI, AJIRA NA UTUMISHI WA UMMA: Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na wanawake na kuwajengea uezo wa kipato wananchi, katika kipindi hiki cha miaka mitano Serikali imeanzisha Mfuko wa Uwezeshaji hapo tarehe 21 Disemba, 2013 ukiwa na jumla ya fedha TZS bilioni 2.413, baada ya kuunganishwa Mfuko wa Kujitegemea, Mfuko wa JK na AK na Mfuko wa Vijana. Kati ya fedha hizo, TZS milioni 973 zilipatikana kwa kuchangishwa kupitia Kamati niliyoiunda, TZS bilioni 1.2 zilitokana na mfuko wa AK/JK na jumla ya TZS milioni 140 ni za Mfuko wa Rais wa Kujitegemea na TZS milioni 100 zilitokana na Mfuko wa Vijana. Lengo kuu kuunda Mfuko wa Kujitegemea ni kuwa na Mfuko ulio imara zaidi katika kuwasaidia vijana, wanawake na vikundi mbali mbali vya wajasiriamali katika shughuli zao za kujiendeleza kiuchumi. Katika kuhakikisha kuwa vijana wanapata fursa za ajira, tumefanikiwa kuzindua Mpango Mkakati wa Ajira kwa vijana wa mwaka 2014/2018. Mpango huu umeweka vipaumbele katika sekta za ujasiriamali, elimu ya amali pamoja na ufundi stadi. Tumepata mafanikio katika kutekeleza Programu ya Ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo kupitia mashamba darasa, shughuli za uvuvi, ufugaji na utalii. Nachukua fursa hii kuwapongeza vijana na wanawake kwa ari na moyo walioonesha katika kuunga mkono jitihada hizi na kwa kutumia vizuri fursa tulizowaandalia. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi hiki cha miaka mitano tumefanikisha kupatikana kwa nafasi za ajira 25,019 Serikalini na katika Sekta Binafsi. Kati ya hizo, nafasi za ajira 4,850 zilikuwa za taasisi mbali mbali za Serikali na nafasi za ajira 20,169 zilitokana na sekta binafsi, zikijumuisha ajira za nje ya nchi na taasisi zinazojitegemea kwa wananchi wa Zanzibar wenye sifa zilizohitajika. Ajira bado ni changamoto nchini kwetu na katika nchi za nje hata zile zilizoendelea. Kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kupambana na tatizo hilo na mipango yetu chini ya mkakati wa ajira unatoa matumaini mazuri. Mheshimiwa Spika, Wakati huo huo, Serikali imefanikiwa kupandisha mishahara ya watumishi wa umma kutoka kima cha chini cha mshahara wa Tsh.100,000 hadi TZS 125,000 kwa mwezi sawa na asilimia ishirini na tano (25%) pamoja na kufanya marekebisho ya mishahara ya wataalamu na wafanyakazi mbali mbali wakiwemo Madaktari, Walimu wa Sayansi na kadhalika. Serikali ilifanya marekebisho hayo ya mwanzo katika mwaka 2011. Vile vile, mwishoni mwa mwaka 2013 na mwanzoni mwa mwaka 2014, Serikali ilipandisha kima cha chini cha mshahara kutoka TZS 125,000 hadi TZS 150,000 sawa na asilimia ishirini (20%) pamoja na kurekebisha mishahara ya watumishi wazoefu, waliotumikia katika utumishi wa umma kwa miaka kumi na tano (15) na zaidi ambao wana mishahara kati ya TZS 150,000 hadi TZS 225,000 katika jitihada za kunyanyua kipato cha mfanyakazi, Serikali imeidhinisha posho mbali mbali ambazo tayari zimeanza kutolewa. Malimbikizo ya mishahara ya walimu yatalipwa kutoka bajeti ya mwaka wa fedha wa 2015/2016 iliyopitishwa na Baraza hili. MIUNDO YA UTUMISHI: Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha utendaji kazi, Serikali imerudisha tena utaratibu wa kuwa na Miundo ya Utumishi katika Mawizara na Taasisi mbali mbali za Serikali. Wizara zote tayari zimeshatengeneza Miundo yao ya Utumishi na zimewasilishwa katika Kamisheni ya Utumishi wa Umma kwa kuthibitishwa. Taasisi nyengine za Serikali yakiwemo mashirika na taasisi zinazojitegemea zimo katika hatua za utayarishaji wa Miundo yao ya Utumishi kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Utumishi wa Umma. Serikali imetoa miongozo mbali mbali kwa ajili ya kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika marekebisho ya mishahara na maposho ili kuhakikisha kwamba hakuna mfanyakazi atakayedhulumiwa haki yake. Mheshimiwa Spika, Vile vile, katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imeimarisha maslahi ya wananchi wanaofanyakazi katika sekta Binafsi kwa kuitaka iongeze mishahara na posho za wafanyakazi wao. Wafanyakazi wa sekta hiyo wameongezewa kiwango cha mishahara yao kutoka TZS 70,000 mwaka 2010 hadi 145,000 kwa sasa, sawa na ongezeko la asilimia 107. Mheshimiwa Spika, Natumia fursa hili kulipongeza Baraza lako Tukufu kwa kupitisha Sheria Namba 2 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011. Sheria hii imetuwezesha kuweka Miundo imara ya uendeshaji na usimamizi wa Utumishi wa Umma na mambo mengine yanayohusiana na hayo. Kutokana na sheria hii, Serikali imeunda Kamisheni ya Utumishi wa Umma pamoja na Tume ya Utumishi Serikalini, Tume ya Utumishi ya Mahakama, Tume ya Utumishi ya Baraza la Wawakilishi na Tume ya Utumishi ya Idara Maalum. Taasisi hizi ni muhimu katika kulinda maslahi na haki za wafanyakazi hapa nchini na zimetoa mchango mkubwa katika kuweka misingi mikuu ya maadili ya Utumishi wa Umma na usimamizi wa rasilimali watu. Jumla ya Sheria za kazi 12 zimetungwa na zimeanza kutumika, zikiwemo kanuni za mwaka 2014 za Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari 2 ya mwaka 2011. Haya yote ni mafanikio ya utekelezaji wa ahadi nilizozitoa za kulinda na kukuza maslahi ya wafanyakazi Serikalini na katika Sekta Binafsi. Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha ustawi wa kinamama na watoto, kuanzia tarehe 21 Aprili 2015 tulianzisha utaratibu unaowawezesha akina mama wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF), kulipwa mafao ya uzazi wanapokwenda kujifungua ili yawasaidie kuimarisha afya zao na za watoto katika kipindi hicho muhimu. Malipo ya mafao ya uzazi hayaathiri malipo ya mafao, ambayo muhusika atapata wakati atakapostaafu. Mheshimiwa Spika, Tunamaliza miaka mitano ikiwa tumo katika hatua za mwisho za kukamilisha Sera ya Usalama na Afya Kazini ili kuweka mfumo mzuri wa afya katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuwakinga wafanyakazi na ajali na majanga mengine yanayotokea katika sehemu za kazi. Aidha, tunamaliza kipindi hiki ikiwa tupo katika hatua za kuanzisha Bima ya Afya. Tumeshafikia hatua nzuri katika kuifikia azma hiyo. SEKTA YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ilitambua kuwa lengo lake la kukuza uchumi wa Zanzibar halitaweza kufanikiwa bila ya azma hiyo kwenda sambamba na uimarishaji wa miundo mbinu ya uchumi kama vile barabara, bandari, viwanja vya ndege, kuimarisha maeneo huru ya uwekezaji pamoja na kuwa na nishati ya uhakika ya umeme. Kwa hivyo, katika kipindi hiki cha miaka mitano, jitihada kubwa zimefanywa katika kuimarisha miundo mbinu hiyo ya uchumi. Mheshimiwa Spika, Kuhusu miundo mbinu ya barabara, Serikali imeendeleza na imekamilisha kazi za ujenzi wa barabara zote kuu zinazoingia mjini. Kadhalika, tumeweza kujenga barabara ndogo ndogo za mijini na mashamba na kuifanya Zanzibar kuwa mfano wa nchi zenye mtandao mzuri wa barabara unaounganisha miji na mashamba na kuwa ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi na kurahisisha shughuli za usafiri wa wananchi na mizigo. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imekamilisha kazi ya ujenzi wa barabara 11 zenye urefu wa (km 102) katika Kisiwa cha Pemba na barabara 4 zenye urefu wa km 34.85 katika Kisiwa cha Unguja. Barabara hizi zimejengwa kwa msaada wa MCC ya Marekani, BADEA na Saud Fund na SMZ. Hivi karibuni tunatarajia kufanya uzinduzi wa barabara ya Wete hadi Gando (km 15) na barabara ya Wete hadi Konde (km 15), ujenzi ambao utakuwa ni suluhisho la tatizo la barabara la muda mrefu lililokuwa likiwasumbuwa wananchi wanaoishi katika maeneo mbali mbali. Kadhalika, kupitia Mfuko wa Barabara Serikali ilikamilisha ujenzi wa barabara ya Amani hadi Mtoni (km 4) na barabara ya njia nne hadi Umbuji yenye urefu wa (km 5). Kazi ya ujenzi wa barabara ya Jendele, kupitia Cheju hadi Unguja Ukuu (km 11.7) na barabara ya Koani hadi Jumbi (km 6.3) kwa msaada wa BADEA unaendelea. Kadhalika, ujenzi wa barabara ya Ole hadi Kengeja yenye urefu wa (km 35) inayojengwa kwa msaada wa OPEC Fund umeshaanza na ujenzi wa barabara kuu kutoka Chake chake hadi Wete unatarajiwa kuanza hivi karibuni. Mheshimiwa Spika, Uimarishaji wa usafiri wa anga ni miongoni mwa masuala yaliyozingatiwa na Serikali ya Awamu ya Saba kama nilivyoahidi wakati wa uzinduzi wa Baraza hili mwaka 2010. Jitihada kubwa zimefanywa katika kukamilisha kazi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ikiwa ni pamoja na ya kurukia ndege, maegesho ya ndege, ujenzi wa uzio, sehemu ya kuegesha magari, ujenzi wa jengo la abiria na kuimarisha huduma mbali mbali zinazohusiana na matumizi ya uwanja huo. Ujenzi wa njia ya kurukia ndege na sehemu ya kuegesha ndege imekamilika na ujenzi wa jengo jipya la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume umefikia hatua nzuri ya utekelezaji ambao tayari umeshafikia asilimia sabini na Oktoba mwaka huu tutakabidhiwa, hii niahadi niliyopewa na uongozi wa Serikali ya China. Mheshimiwa Spika, Kuhusu kiwanja cha ndege cha Pemba, Serikali inaendeleza mipango mbali mbali kwa ajili ya kukiimarisha kiwanja hiki ili kiweze kutumika usiku na mchana na baadae kiweze kutumiwa na ndege zilizo kubwa zaidi. Katika juhudi tunazoendelea kuchukua za kuimarisha kiwanja hicho, tarehe 16 Machi 2015 Serikali iliingia mkataba na Kampuni ya Safegate ya Ujerumani kwa ajili ya uletaji wa vifaa pamoja na kusimamia uwekaji wa taa katika kiwanja kwa gharama ya Dola za Kimarekani 508,219.45. Hivi sasa, Kampuni hiyo imeshalipwa malipo ya awali ya aslimia 20. Vifaa mbali mbali kwa ajili ya uwekaji taa hizo vimeshafika Pemba na kazi ya uchimbaji misingi kwa ajili ya kulaza nyaya imeanza. Kwa upande wa usimamizi wa “civil work” mtaalamu wa Kampuni hiyo tayari amewasili katika kiwanja cha ndege cha Pemba kusimamia kazi ya uchimbaji misingi na mashimo. Kazi ya uwekaji taa inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa Julai. Sambamba na juhudi hizi Serikali, inaendelea kufanya mazungumzo na washirika wa maendeleo mbali mbali ili kupata fedha kwa ajili ya kuimarisha zaidi Uwanja wa Ndege wa Pemba. Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imekubali kufadhili kazi ya Upembuzi Yakinufu na mpango mkuu wa kiwanja hicho; kazi ambayo inatarajiwa kuanza ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo. Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia sana katika jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuitangaza Pemba katika masoko ya utalii duniani na kuimarisha biashara na huduma za usafiri kwa wananchi wa Unguja na Pemba. Mheshimiwa Spika, Serikali imezingatia umuhimu wa bandari, kwa hivyo kwa kushirikiana na Kampuni ya Azam Marine imejenga majengo mapya ya kupumzikia abiria katika Bandari ya Malindi. Aidha, vifaa mbali mbali vimenunuliwa ili kuongeza ufanisi na kasi ya upakiaji na uteremshaji wa mizigo katika meli zinazofika Bandari ya Malindi. Serikali vile vile imeifanyia matengenezo makubwa gati ya Mkoani Pemba ili kurahisisha shughuli za usafiri wa vyombo na abiria wanaoitumia bandari hiyo. Ujenzi wa gati ya Tumbatu unaendelea na ujenzi wa gati ndogo ya Mkokotoni unategemewa kuanza katika mwaka wa fedha, 2015/2016. Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa nafasi katika Bandari ya Malindi na kuwa na Bandari ya kisasa yenye huduma bora zaidi, tayari Serikali imeanza hatua za awali za ujenzi wa Bandari mpya ya Mpiga duri. Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imekubali kushirikiana nasi katika ujenzi huo kupitia Benki ya Exim ambapo hatua ya Upembuzi Yakinifu zimeshafanywa na Kampuni ya Chec ya China ndio itakayojenga bandari hio kwa kushirikiana na Serikali. Mheshimiwa Spika, Tumefikia hatua nzuri katika kutekeleza Ujenzi wa bandari hiyo ambao ulibuniwa kabla ya mwaka 2000 wakati wa uongozi wa Dk. Salmin Amour Juma. Serikali imepanga kujenga Bandari hiyo kubwa na ya kisasa ili Zanzibar iweze kwenda sambamba na mabadiliko ya biashara na uchumi yanayotokea duniani. Bandari hii mpya itahudumia meli zenye uzito wa Tani 50, 000 (Deadweight tonnage) na itakuwa na urefu wa mita 300 na upana wa mita 490. Ujenzi wa bandari hio utaanza mara tu baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo jipya la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (Terminal 2). Kwa lengo la kuimarisha usafiri wa baharini, Serikali iliamua kujenga Meli ya abiria na mizigo ili kupunguza tatizo kwa wananchi na wafanyabiashara. Meli hiyo inayojengwa katika Jamhuri ya Korea inayotarajiwa kufika nchini katika mwezi wa Julai, 2015 ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na mizigo yenye uzito wa tani 200. Mheshimiwa Spika, Nishati ya umeme ni muhimu katika kuimarisha ukuaji wa uchumi wa nchi na ustawi wa maendeleo ya wananchi wetu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika awamu zake mbali mbali imefanya jitihada kadhaa za kuhakikisha Zanzibar inakuwa na huduma ya nishati ya umeme ya uhakika. Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, tumeweza kukamilisha hatua hizo zilizoanzishwa na Awamu ya sita za kuwa na umeme wa MW 100 kwa Unguja na MW 20 kwa Pemba, viwango ambavyo ni zaidi ya mahitaji halisi ya nishati hiyo kwa sasa. Katika hotuba ya tarehe 11 Novemba, 2010 nilipolizinduwa Baraza la nane, niliahidi kuwa Serikali itapeleka umeme katika maeneo yote ambayo bado hayajapata nishati hiyo ikiwa ni pamoja na kisiwa cha Makoongwe, Kisiwa Panza na Kisiwa cha Shamiani huko Pemba. Utekelezaji wa azma hii umefikia hatua ya kuridhisha. Nina furaha kuelezea mafanikio makubwa ambayo Serikali imeyapata katika utekelezaji wa usambazaji wa umeme. Hivi sasa huduma za umeme zinapatikana katika miji yote na zimefikia zaidi ya vijiji 129 badala 123 vilivyokadiriwa mwanzo. UCHIMBAJI WA MAFUTA NA GESI: Mheshimiwa Spika, Nimefurahi kuona kuwa Baraza hili la Nane limejadili kwa kina suala la uchimbaji wa mafuta na gesi na mmeweza kutoa michango na kuishauri Serikali kwa namna mbali mbali kuhusiana na suala hili. Hivi sasa tumefikia pazuri hasa tukizingatia kuwa Katiba Inayopendekezwa imezingatia matakwa ya Zanzibar juu ya suala hili. Katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imefanya mazungumzo na kusaini makubaliano ya Awali na Kampuni zinajishughulisha na uchimbaji mafuta, ikiwemo Kampuni ya RAK Gas ya Ras Al Khaima kufuatia ziara yangu ya mwaka 2012 na kampuni ya Shell kufuatia ziara ya Uholanzi niliyoifanya mwezi Agosti, 2013. Dhamira yetu ni kuona kuwa katika kipindi kifupi kijacho mafuta na gesi yanachimbwa Zanzibar baada ya kufanyiwa kazi masuala ya kisheria. HUDUMA ZA JAMII: Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ilitambua wazi kuwa kuimarisha huduma za jamii ni jukumu lake la msingi na hatua muhimu ya kuendeleza shabaha ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imechukua jitihada mbali mbali katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Elimu, Afya na Maji Safi na Salama katika maeneo yote ya Unguja na Pemba, mijini na mashamba. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa sekta ya elimu, niliahidi kuendeleza mafanikio ya elimu yaliyopatikana katika Awamu zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizotangulia. Kadhalika, Serikali yangu iliweka azma ya kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi zote kuanzia Maandalizi, Msingi, Sekondari, Elimu ya Juu pamoja na Mafunzo ya Elimu Amali na Elimu Mbadala. Pamoja na hatua hizo, tulidhamiria kuimarisha masomo ya sayansi hasa kwa watoto wa kike, mafunzo ya elimu maalum kwa watu wenye ulemavu, kuimarisha maslahi ya walimu pamoja na kuyaimarisha mazingira ya kusomea yakiwemo majengo na vifaa vya maabara na vitabu vya kiada na ziada. Mheshimiwa Spika, Ni jambo la kufurahisha kuona mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imeweza kuyapata katika utekelezaji wa malengo hayo niliyoyabainisha ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2010 – 2015 na mipango mingine ya Kitaifa niliyoitaja hapo awali. Wakati tukiwa katika mwaka wa tano wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, tunafarajika kwa mafanikio ya kuandikisha watoto wote waliofikia umri wa kusoma. Serikali imeondoa michango ya wazazi katika elimu ya msingi na kuondoa gharama za mitihani yote ya Sekondari kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 ili kuwawezesha watoto wote kupata elimu bila ya malipo kwa shabaha ile ile ya tamko la Mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alilolitangaza tarehe 23 Septemba, 1964. Katika kipindi hiki cha miaka mitano, tunajivunia kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya lazima; Maandalizi, Msingi na Sekondari kutoka jumla ya wanafunzi 317,278 mwaka 2010 hadi kufikia wanafunzi 390,464 mwaka 2015. Mheshimiwa Spika, Serikali imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa mradi wa uimarishaji wa elimu ya lazima kwa kutumia fedha zetu na michango ya washirika wa maendeleo kwa kujenga majengo mapya ya skuli, kununua vifaa vya maabara na samani. Serikali imeweza kushirikiana vyema na wananchi pamoja na sekta binafsi katika kuongeza nafasi na fursa za kupata elimu kwa watoto wa Zanzibar na kupanua wigo wa mafunzo yanayotolewa katika elimu ya juu hususan katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Kadhalika, Serikali iliendelea kuchukua hatua ya kuwapatia mikopo vijana wanaojiunga na taasisi za elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Zanzibar. Idadi ya skuli zimeongezeka. Skuli za maandalizi sasa ni 270 kutoka 238 mwaka 2010. Skuli za msingi zimeongezeka kutoka 299 mwaka 2010 hadi skuli 370 mwaka 2015. Serikali inajiandaa kujenga skuli mpya 10 za ghorofa ili kuongeza nafasi kwa wanafunzi. Ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, Serikali inatekeleza mradi wa Tz – 21 unaohusiana na masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika skuli za msingi 248. Skuli hizo zimepatiwa vifaa mbali mbali ikiwa ni pamoja na Kompyuta, Vitabu na Vifaa vyengine vya ufundi wa TEHAMA pamoja na kuwapatia mafunzo watendaji wanaosimamia mradi huo. Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza hili, niliahidi kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha Elimu ya Sekondari kwa kuchukua hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuyaimarisha mazingira ya ufundishaji na usomaji kwa kuwapatia walimu mafunzo, kujenga Skuli mpya 21 ili kuongeza nafasi, kuzifanyia matengenezo makubwa skuli sita za sekondari na kuzipatia vitabu na vifaa vya maabara skuli zetu pamoja na samani. Kadhalika, kwa lengo la kuwashajihisha watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi, niliahidi kuanzisha skuli maalum za sekondari kwa ajili ya watoto wa kike, ambapo skuli ya sekondari ya Ben Bella kwa Unguja na skuli ya Utaani kwa Pemba tayari zimeshaanzishwa kwa lengo hilo. Idadi ya Skuli za Sekondari kuanzia kidatu cha kwanza hadi cha Sita imeongezeka kutoka skuli 194 mwaka 2010 hadi skuli 263 mwaka 2015. Serikali imeweza kukamilisha azma yake ya kuzifanyia matengenezo makubwa Skuli sita za zamani za Sekondari za Unguja na Pemba na kuzipatia vifaa vya maabara na samani kama ilivyoahidiwa. Aidha, tumeweza kukamilisha ujenzi wa Skuli mpya za Sekondari 19 kama tulivyoahidi na tayari skuli hizo zinatumika. Serikali imechukua jitihada maalum katika kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata haki yao ya elimu katika skuli zetu mbali mbali, kupitia mpango wa elimu mjumuisho, pamoja na kuyaimarisha mafunzo ya elimu ya amali na ufundi katika vituo vya Mwanakwerekwe, Mkokotoni na Vitongoji. Vituo hivi vimetoa mchango mkubwa wa kuwapatia vijana wetu mafunzo mbali mbali ya fani za ufundi zikiwemo uashi, useremala, ushoni, uhunzi, upishi, uchoraji, ufundi bomba, ufundi umeme, magari, mafriji, teknolojia ya habari na fani nyenginezo. Mheshimiwa Spika, Mafanikio makubwa yamepatikana katika kuimarisha fursa za elimu ya juu nchini ili kwenda sambamba na mahitaji ya wataalamu wetu wenyewe. Wanafunzi waliojiunga katika vyuo vikuu vitatu vya Zanzibar; imeongezeka kutoka vijana 3,624 mwaka 2010 na kufikia 6,367 mwaka 2015. Mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la masomo katika viwango mbali mbali kuanzia Ngazi ya Cheti hadi Shahada ya Uzamivu (PhD). Katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika kipindi hiki, idadi ya skuli za masomo (faculties) imeongezeka kutoka moja hadi tano. Kadhalika, chuo hiki tayari kimeanza benchi ya pili ya Shahada ya Uzamivu ya Kiswahili pamoja na kuanzisha kitivo cha masomo ya udaktari (Faculty of Medicine) katika mwaka 2013. Jambo kubwa zaidi ni ongezeko la wasichana katika masomo ya juu. Katika Mahafali ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) mwaka 2014, idadi ya wahitimu wa kike ilikuwa ni asilimia 64 kati ya wahitimu 741 wa chuo hicho. Mwaka huu wa 2015 chuo kina wanafunzi 2705 ambapo 1654 ni wanawake na 1051 ni wanaume. Hayo ni miongoni mwa mafanikio ambayo nchi yetu inapaswa kuyaendeleza. Mheshimiwa Spika, Kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanaopata fursa ya elimu ya juu wanaendelea na masomo yao, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa mikopo kila mwaka kwa wanafunzi wapya na wale wanaoendelea. Hadi kufikia mwezi Disemba, 2014 wanafunzi 4,678 walipewa mikopo yenye thamani ya TZS bilioni 19.4. Katika mwaka wa fedha 2014/2015. Serikali ilipanga kutoa udhamini kwa wanafunzi wapya wa elimu ya juu 1,200. Hata hivyo, idadi halisi iliongezeka hadi kufikia wanafunzi 1,611 sawa na ongezeko la asilimia 34 ya malengo. Mheshimiwa Spika, Uimarishaji wa huduma za afya nchini ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi, Awamu ya Saba na Shabaha ya Mapinduzi ya mwaka 1964. Miongoni mwa jukumu la msingi la Serikali lilikuwa ni kuyaendeleza mafanikio ya Sekta ya Afya ya Awamu za Serikali zilizopita na kutekeleza mikakati ya mipango ya Kitaifa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, MKUZA II, Dira ya 2020 na Malengo ya Milenia pamoja na kuhakikisha Sera ya Afya inatekelezwa kwa vitendo kwa kushirikiana na wananchi. Miongoni mwa malengo makuu ya Serikali yalikuwa ni kuimarisha huduma za Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ili ifikie kuwa Hospitali ya Rufaa, kuiimarisha Hospitali ya Abdalla Mzee na Hospitali ya Wete ili zifikie hadhi ya kuwa Hospitali za Mkoa. Kwa upande wa Hospitali ya “Cottage” ya Kivunge na Makunduchi kwa Unguja na Micheweni na Vitongoji kwa Pemba, Serikali ilikusudia zifikie hadhi ya Hospitali za Wilaya. Hospitali ya Koteji ya Makunduchi imepiga hatua mbele zaidi. Malengo mengine ni kuanzisha Vitengo vya matatizo ya Figo, Maradhi ya Moyo na Saratani ili huduma hizo ziweze kupatikana nchini pamoja na kuziimarisha huduma za kinga na tiba. Mheshimiwa Spika, Mabadiliko makubwa yamefanywa katika kipindi cha miaka mitano katika kuimarisha mazingira na huduma zinazotolewa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ili ifikie hadhi ya Hospitali ya Rufaa. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuipatia Hospitali hiyo vifaa vya kisasa katika Chumba cha Upasuaji, Maabara ya Uchunguzi wa maradhi, Wodi ya Wagonjwa Mahatuti, Wodi ya Wazazi na Chumba cha Wagonjwa wa dharura. Jengo jipya la huduma za upasuaji wa Kichwa na Uti wa Mgongo limefunguliwa likiwa ni la huduma za aina yake katika Afrika ya Mashariki. Kituo cha Meno cha Tabasam kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye matatizo ya midomo nacho kimeanzishwa. Vile vile, Serikali imeanzisha Kitengo cha uchunguzi wa maradhi ya mfumo wa chakula pamoja na Wodi mpya ya Wagonjwa Mahututi. Hivi sasa, Serikali inaendelea na mradi wa ujenzi wa jengo jipya la watoto ambalo pia litakuwa na huduma za wagonjwa wa maradhi ya figo. Ni jambo lililo wazi kuwa huduma katika Hospitali ya Mnazi Mmoja zimeimarika sana na zimepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wagonjwa ambao walikua wakifuata baadhi ya huduma nje ya Zanzibar. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi mkubwa wa Hospitali ya Abdalla Mzee kwa kuiwekea miundo mbinu ya kisasa na vifaa ili iweze kukidhi kuwa Hospitali ya Rufaa Pemba. Katika Hospitali ya Wete, huduma zimeimarishwa za shughuli za uchunguzi wa maradhi mbali mbali, ujenzi wa jengo la maabara mpya umekamilika. Wodi mpya ya wazazi, wodi ya wagonjwa wa akili na chumba cha upasuaji zimejengwa. Mheshimiwa Spika, Mwamko wa wananchi juu ya elimu ya afya na jitihada za Serikali katika kuimarisha huduma hizo kumechangia sana katika kuongezeka kwa asilimia ya mama waja wazito wanaojifungua katika vituo vya afya hadi kufikia asilimia 68.3 mwaka 2014. Hivi sasa huduma za kujifungua zinapatikana bure katika vituo 41 nchini. Vifo vya watoto wanaozaliwa hai chini ya umri wa mwaka mmoja vimepungua kutoka 54/1000 mwaka 2010 hadi 46/1000 mwaka 2012 zaidi ya lengo lililokuwepo la vifo 48/1000. Vile vile kuna mafanikio katika kupunguza vifo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 kutoka 73/1000 mwaka 2010, 66/1000 mwaka 2012. Lengo ni kufikia 50/1000. Vifo vya kinamama kutokana na uzazi vinazidi kupungua. Kadhalika, Serikali imeendelea kudhibiti kiwango cha Malaria na VVU/UKIMWI kuwa chini ya asilimia moja. Kwa mujibu wa tathmini ya kiwango cha maambukizo ya VVU, Zanzibar inakisiwa kuwa na asilimia 0.5 ya maambukizi kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24, asilimia 0.6 kwa wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49. Katika kipindi hiki Serikali imejenga ghala la kisasa la kuhifadhia dawa katika eneo la Maruhubi. Serikali za Marekani na Denmark zimesaidia ujenzi huu. Vile vile, Ofisi ya Mkemia Mkuu hivi sasa imehamishiwa katika eneo hilo ili kupata fursa ya kufanya shughuli zake katika mazingira yaliyo bora zaidi. Mheshimiwa Spika, Jitihada kubwa zimefanywa katika kukiimarisha Chuo cha Taaluma ya Sayansi za afya. Mafanikio yamepatikana ambapo kwa sasa idadi ya madaktari wazalendo imefikia 102. Tunategemea idadi hiyo itaongezeka hasa baada ya Serikali kuamua kuanzisha mafunzo ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na wanafunzi wanaosomea udaktari Tanzania Bara na nje ya nchi. Kwa wastani daktari mmoja alikuwa akihudumia wagonjwa 31,838 (1:31,838) mwaka 2010 na ambapo sasa anahudumia wastani wa wagonjwa 18,810 (1:18,810). Pamoja na madaktari wazalendo, wapo madaktari wa kigeni 20 kutoka China na 20 kutoka Cuba. Idadi hii inafanya madaktari wote kuwa 151 ambapo wastani wa daktari mmoja anahudumia watu 9,093 (1:9,093). Napenda nitoe shukurani zangu kwa washirika wetu wa maendeleo wanaotuunga mkono katika azma yetu ya kuziimarisha huduma za afya nchini. Tunathamini sana misaada yao ya mafunzo na utaalamu, vifaa, wafanyakazi na nyenzo mbali mbali ambazo kwa pamoja zimeweza kutuletea mafanikio tuliyoyapata. Zanzibar ina mtandao mzuri wa huduma za afya zinazotolewa katika hospitali na vituo vya afya vya Serikali, Vikosi vya Ulinzi, Taasisi za Kijamii na vituo vya watu binafsi kuliko nchi nyingi. Katika Bara la Afrika; mwananchi wa Zanzibar hatembei umbali wa kilomita tano, bila ya kupata huduma za afya kwenye kituo cha afya. MAJI SAFI NA SALAMA: Mheshimiwa Spika, Wakati nikilifungua Baraza hili, nilisema kuwa maji ni uhai na hasa maji safi na salama. Kwa hivyo, Serikali yangu imeendeleza jitihada za Serikali za Awamu zilizopita na kuweka mikakati mipya katika kuwapatia wananchi huduma za maji safi na salama. Mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ni pamoja na kukamilisha mradi wa usambazaji wa maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi, kupunguza upotevu wa maji na kuvihifadhi vianzio vya maji. Katika ahadi zangu nilibainisha kuwa kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015, Serikali inakusudia kusambaza huduma za maji safi na salama kufikia asilimia 95 kutoka asilimia 75 katika miji na asilimia 80 kutoka asilimia 60 katika vijiji ifikapo mwaka 2015. Hali ya uzalishaji wa maji imefikia lita milioni 17.6 ambayo imewezesha kuongezeka kwa watu wanaopata maji na kufikia 175,873 katika kipindi hiki. Mahitaji yetu halisi ya maji ni lita milioni 214.6 ambapo uzalishaji katika kipindi hiki umefikia lita milioni 163 sawa na asilimia 76 ya mahitaji. Kutokana na takwimu hizi upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi umefikia asilimia 87.7, Mkoa wa Kusini Unguja asilimia 76.45, Mkoa wa Kaskazini Unguja asilimia 71.68, Mkoa wa Kusini Pemba asilimia 74.08 na Mkoa wa Kaskazini Pemba asilimia 56.42 ya mahitaji halisi. ARDHI NA MAKAAZI: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kushughulikia suala la matumizi bora ya ardhi kwa kuzingatia udogo wa ardhi tuliyonayo. Katika utekelezaji wa azma hii, Serikali imetayarisha sera mpya ya ardhi ili kusimamia na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi. Sera hiyo pamoja na mambo mengine imezingatia mabadiliko ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi yaliyopo na yatakayokuja baadae. Kazi ya usajili wa ardhi imeshafanywa katika zaidi ya shehia 20 na zoezi la utambuzi linaendelea katika shehia 13. Jumla ya nyumba, viwanja na mashamba 22,398 vimeshatambuliwa sambamba na hatua hiyo, zoezi la utoaji wa Hati za matumizi ya Ardhi linaendelea kwa kutoa hati mpya na kuzibadilisha zile za zamani. Hadi sasa jumla ya mikataba ya matumizi ya ardhi 223 imeshasainiwa na kukabidhiwa wawekezaji. Vile vile, hati 1,310 za matumizi mbali mbali ya ardhi zimetolewa na viwanja 1,691 vimepimwa, Unguja na Pemba. Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na tatizo la matumizi mabaya ya ardhi, Serikali imeshakamilisha mpango mkuu wa matumizi ya Ardhi ya Mji wa Zanzibar na Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Ardhi Zanzibar, sambamba na mipango ya matumizi ya ardhi ya Mikoa yote ya Zanzibar. Katika kuhakikisha uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar, Serikali imeanzisha mfumo mpya kwa njia ya kuishirikisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kwa ajili ya kuhifadhi nyumba ziliopo Mji Mkongwe. Mfumo huo utafanywa kupitia Kampuni itakayoitwa Hifadhi Zanzibar na tayari imeshasajiliwa na kuanza kazi zake. Aidha, Serikali inaendelea na matayarisho ya kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Miji ili kusimamia ustawi wa maendeleo ya miji yetu. Nina matumaini makubwa kuwa kupitia mipango hiyo, wananchi wataelimika na watazidi kuifahamu mipango ya matumizi bora ya ardhi na utaratibu huu utapunguza changamoto zilizopo hivi sasa. Nawasihi sana wananchi waendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango hii ili tuweze kufikia azma yetu ya matumizi bora ya ardhi. HABARI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa habari, katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imeimarisha utoaji wa habari kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kurusha moja kwa moja matangazo yanayohusu vikao vya Baraza la Wawakilishi. Tumeliwezesha Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kufanya mageuzi ya kutoka mfumo wa "Analogue" kwenda "Digital" kwa mafanikio na kwa wakati tuliopangiwa na Jumuiya za Kimataifa. Tumeongeza muda wa kutangaza, ambapo hivi sasa ZBC Radio na TV zinakuwa hewani kwa saa 24. Vile vile, gazeti la Zanzibar Leo linalotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ubora wake wa habari na uchapishaji umeongezeka na hivi sasa linapatikana kila siku katika maeneo mbali mbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Zanzibar imepiga hatua kubwa kwa kuongeza idadi ya vyombo vya habari zikiwemo radio jamii 4 pamoja na vituo vya habari binafsi. Hali hii imechangia sana kuongezeka kwa uhuru wa kupata habari na kusukuma maendeleo ya jamii yetu katika nyanja mbali mbali. Vile vile, Serikali imetekeleza azma yake ya kuwajengea wasanii wetu “Studio” za kisasa za kurekodia nyimbo na michezo ya kuigiza kwenye jengo la zamani la Utangazaji la Sauti ya Tanzania Zanzibar, baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa. Mheshimiwa Spika, Kwa lengo la kutekeleza azma ya Serikali ya kukifufua Kiwanda cha Upigaji Chapa na Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ili kurudisha hadhi yake na kuinua kiwango cha uzalishaji, jumla ya TZS milioni 5,532.40 zimetumika kwa matengenezo ya majengo yaliyokuwa kiwanda cha sigara Maruhubi pamoja na ununuzi wa mashine mpya za kisasa za uchapishaji za kiwanda hicho. Serikali ina lengo la kukiimarisha zaidi ili kiweze kuchapisha magazeti, vitabu vikubwa na kadhalika. Fedha kwa ajili ya kazi hio tayari zimepatikana kutokana na msaada wa Serikali ya Oman. Ni dhahiri kukamilika kwa kiwanda hiki kumeipunguzia mzigo Serikali na kitaiwezesha kutoa huduma zenye ubora wa kiwango kikubwa zaidi. Mheshimiwa Spika, Kwa lengo la kuziimarisha huduma za mawasiliano Serikalini, katika kipindi hiki cha kwanza cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, Serikali imeanzisha mradi wa “e-go
Official Reports
MUONGOZO WA KUOMBA KIBALI CHA UTAFITI-Date Posted: 17-09-2018
FOURTH SCHEDULE (KIAMBATANISHO)-Date Posted: 17-09-2018
RESEARCH/FILMING APPLICATION FORM -Date Posted: 17-09-2018
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO MHE. DKT. KHALID SALUM MOHAMED KUHUSU MAPENDEKEZO YA BAJETI YA SERIKALI (MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI) KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018 -Date Posted: 25-07-2018
RATIBA YA MKUTANO WA KUMI WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI UTAKAOJADILI BAJETI YA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019-Date Posted: 10-05-2018

Research

Procedure
Research in Zanzibar
Publications
Conferences
PROJECTS

Ongoing Projects
Upcomming Projects
Previous Projects
Reports in Projects
Publication from Projects
GALLERY

Government Activies
Kilimo