Drop Down Menu
FOR VISITORS
Tourism
Work in Zanzibar
Investment
Business
Study in Zanzibar
Immigration

FOR CITIZEN
Travel Documents
Zanzibar ID
National ID
Social Security
Driving Licence
Health System
E-Government
Zanzibar Port
Municipality

Quick Links
Ikulu Zanzibar
Tanzania
Baraza la Wawakilishi
Bunge Tanzania
Zanzibar Electoral Commission
National Electoral Commission

Zanzibar
Zanzibar
Government News Highlights
Hutuba ya Rais wa Zanzibar na MBM Mhe:Dk.Ali Mohamed Shein baada ya kuapishwa
HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, BAADA KUAPISHWA KUWA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, UWANJA WA AMAAN TAREHE 24 MACHI, 2016 Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi Wakuu Wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waheshimiwa Mawaziri Mheshimiwa Job Ndugai; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Othman Chande Mohamed; Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Omar Othman Makungu; Jaji Mkuu wa Zanzibar, Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Mheshimiwa Abdulrahman Kinana; Katibu Mkuu wa CCM, Viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya Siasa mliopo, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Wageni Waalikwa, Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana, Assalam Aleikum, 2 Kwa hakika, sifa njema zote anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu; Subhana Wataala; Muumba wa Mbingu na Ardhi; ambaye kwa uwezo wake ameturuzuku neema ya uhai na uzima, tukaweza kuifikia siku hii, baada ya wananchi wa Zanzibar kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa marudio uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016 kwa amani na salama. Tuna wajibu wa kumshukuru Mola wetu Mtukufu mwingi wa Rehema, ambaye humpa madaraka amtakaye. Kwa uwezo wake, tumeweza kuifikia hatua hii muhimu ya kidemokrasia na maendeleo kwa nchi yetu tukiwa katika hali ya salama, amani na umoja. Naipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kwa kuyafanikisha majukumu yake ya kikatiba ya kuandaa na kusimamia Uchaguzi Mkuu uliorudiwa tarehe 20 Machi, 2016 na matokeo ya kura za Urais kutangazwa tarehe 21 Machi, 2016. Kadhalika, natoa shukurani kwa waangalizi wa Uchaguzi, kutoka ndani na nje ya nchi ambao walikuwepo nchini kwa shughuli za uangalizi. Ushiriki wao, hapana shaka, utabainisha jinsi uchaguzi wetu ulivyofanyika kwa misingi ya haki, uhuru, amani na utulivu. Ndugu Wananchi, Natoa shukurani kwa Chama changu cha Mapinduzi, kuanzia Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa, Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na Jumuiya zote za CCM, kwa kuniamini na kuniteua niwe mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa kipindi chengine cha miaka mitano. Naiheshimu na naithamini fursa hii adhimu niliyopewa na Chama chetu. Nafahamu kuwa, Chama cha Mapinduzi kina hazina kubwa ya wanachama wenye uwezo wa kuongoza, lakini kwa hekima na busara za viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali, Chama kiliamua, kwa makusudi, kunichagua mimi ili niendelee kuipeperusha bendera ya Chama chetu kwa nafasi hiyo. Ushirikiano nilioupata, kutoka kwa viongozi na wanachama wa CCM tangu hatua za awali hadi siku iliyotangazwa matokeo, umenitia moyo na kuniongezea ujasiri. Bila ya shaka, sote kwa pamoja tumeyafurahia matokeo ya ushindi wa kishindo tulioupata, kwani hayo ndio matunda ya juhudi ya kazi kubwa tuliyoifanya sote kwa pamoja kwa kipindi kirefu. 3 Shukurani zangu, ziwaendee viongozi na wanachama wa CCM, wapenzi wa CCM na wananchi wanayoyapenda maendeleo ya Zanzibar, katika ngazi zote kwa kushiriki katika kukipatia ushindi mkubwa Chama cha Mapinduzi. Kazi yetu, hiyo ya pamoja, imelinda heshima ya CCM na kuendeleza matumaini waliyonayo wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa jumla juu ya uwezo wa Chama hiki kikubwa chenye uzoefu wa siasa wa muda mrefu. Kadhalika, hatua hiyo imetuwezesha kushinda na kufikia lengo la kuiongoza nchi yetu. Hongereni sana Wana-CCM na Wazanzibari wote kwa chaguo sahihi. Nasema ahsanteni sana. Ndugu Wananchi, Natoa shukurani zangu za dhati, kwenu wananchi kwa kujitokeza kwa wingi sana kuitumia haki yenu ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wenu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Kujitokeza kwenu kwa wingi kupiga kura tarehe 20 Machi, 2016, kwa idadi kubwa ni kielelezo cha kukomaa kwenu kisiasa na kidemokrasia na kutambua kuwa uchaguzi ulio huru na haki, ndio njia sahihi ya kuwapata viongozi wa nchi yetu kwa misingi ya Sheria na Katiba. Nakupongezeni kwa kuitumia vizuri haki yenu hiyo ya kuwachagua viongozi watakaoiongoza nchi yetu katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Hongereni sana. Vile vile, natoa shukurani zangu za dhati kwenu, kwa kunichagua kwa kura zenye asilimia 91.4, nikiwa Mgombea niliyesimamishwa na CCM. Ushindi tulioupata umeniwezesha kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kuwa mshindi wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, kwa kipindi chengine cha miaka mitano, kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa Tume hiyo na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Ndugu Wananchi, Kadhalika, kuwachagua wagombea wenzangu, wa Chama cha Mapinduzi, katika nafasi za Uwakilishi na Udiwani na wabunge waliochaguliwa awali ni kielelezo cha imani kubwa mliyonayo kwa Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya kuiongoza nchi hii na kuleta maendeleo zaidi kufuatana na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015/2020. Sote, tunathamini sana heshima mliyotupa. Nasi tutahakikisha 4 tunatimiza wajibu wetu ipasavyo kwa kukutumikieni katika kuziinua hali za wananchi ili ziwe bora zaidi. Ndugu Wananchi, Kwa mara nyengine tena, nawapongeza wagombea wenzangu wa nafasi ya Urais kwa kuyakubali matokeo ya uchaguzi na kuyaheshimu maamuzi ya wananchi. Kadhalika, natoa shukurani kwao kwa kuniahidi mbele ya wananchi siku ya tarehe 21 Machi, 2016, kwenye ukumbi wa Salama katika hoteli ya Bwawani juu ya dhamira yao ya kushirikiana na Serikali nitakayoiunda, katika kuwatumikia wananchi na kuijenga nchi yetu. Kwa hakika nimepata imani kubwa kutokana na maelezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed, kwa niaba ya vyama mbali mbali vilivyoshiriki katika Uchaguzi. Kauli yao ya pamoja, imenipa moyo na matumaini makubwa ya kushirikiana na vyama hivi katika kuendelea kuijenga Zanzibar. Kwa upande wangu, nachukua nafasi hii kuwaahidi kwamba nitashirikiana nao katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar, kwa manufaa yetu sote, bila ya ubaguzi wa aina yoyote; kwani mimi ni Rais wa wananchi wote wa Zanzibar. Nitaongoza kwa kuzingatia Katiba ya Zanzibar na nitatenda haki bila ya kumdhulumu yeyote. Ndugu Wananchi, Navipongeza sana vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama vya SMT na Idara Maalum za SMZ, kwa kuhakikisha kuwa nchi yetu imeendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu kwa kipindi chote cha miaka mitano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba. Katika kipindi hicho, vikosi vyetu vimefanya kazi nzuri ya kuilinda nchi yetu na kuhakikisha kuwa wananchi na wageni wanaoitembelea nchi yetu wapo katika hali ya amani wakiendelea na shughuli zao bila ya usumbufu. Tanzania ipo salama na ina amani. Zanzibar nayo ipo salama na ina amani. Natoa shukurani zangu kwenu wananchi, kwa kupiga kura na kusherehekea ushindi kwa utulivu, kwa misingi ya kudumisha amani na utulivu. Hili ni jambo kubwa na la msingi kwani uchaguzi ni mchakato wa muda tu, kwa ajili ya kuwapata viongozi wa ngazi mbali mbali katika nchi yetu lakini amani na utulivu ni masuala ya kudumu. Hongereni sana. 5 Ndugu Wananchi, Kusimamia na kudumisha amani itakuwa ndio kipaumbele cha Serikali nitakayoiunda. Nitatumia uwezo wangu wote na nitafanya kila jitihada ili kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaendelea kudumu, nikiamini kwamba hakuna mbadala wa amani na ndio msingi muhimu katika kuufanikisha utekelezaji wa mipango yetu ya kazi kwa kuzingatia Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2015/2020. Kwa mnasaba huo, Serikali zote mbili hazitomvumilia mtu yoyote au kikundi chochote kitakachofanya vitendo vinavyoashiria uvurugaji wa amani na utulivu wetu. Ni wajibu wa kila mmoja wetu auone umuhimu wa kuitunza na kuiendeleza amani. Ni jukumu la viongozi wote wa Serikali, wanasiasa, viongozi wa madhehebu ya dini, viongozi wengine katika jamii na wananchi wote kutekeleza wajibu wetu na kuhakikisha tunadumisha amani na utulivu na tunafuata sheria. Vile vile, shukurani zangu, nazitoa kwa viongozi wa dini wa madhehebu yote kwa nyakati mbali mbali ambao waliendelea kuhubiri na kutukumbusha umuhimu wa kuitunza amani pamoja na kuiombea dua nchi yetu wakati wote. Ndugu Wananchi, Kadhalika, nautambua na nauthamini mchango wa vyombo vya habari katika kuwapa habari za matukio mbali mbali ya uchaguzi wananchi na kuwashajihisha juu ya umuhimu wa kuitumia haki yao ya kidemokrasia kushiriki katika kupiga kura. Aidha, natoa shukurani kwa vikundi vyetu vya sanaa na burudani ambavyo tulishirikiana navyo katika hatua mbali mbali, na mchango wao katika kuhimiza amani na utulivu nchini. Vilifanya kazi kubwa na nzuri. Ninachowaahidi ni kuendelea kushirikiana navyo, kwani mchango wao ni muhimu katika kuyahamasisha maendeleo ya nchi yetu. Natoa shukurani zangu maalum kwa mke wangu, Bibi Mwanamwema Shein na wana familia yangu wote, marafiki zangu, wasaidizi wangu wote na wana CCM wenzangu kwa mchango wao, nasaha zao, busara, hekima na dua zao hadi kufikia hatua hii ya 6 kuapishwa kwangu, kuiongoza nchi yetu kwa kipindi chengine cha miaka mitano. Napenda nikuahidini wananchi nyote kuwa nitaunda Serikali itakayozingatia umuhimu wa kuwaunganisha wananchi wote, kuyaendeleza mafanikio yote yaliyokwishapatikana na kuimarisha misingi ya sheria na utawala bora. Vile vile, nitahakikisha kwamba malengo makuu ya Mapinduzi yetu ya tarehe 12 Januari, 1964 yanadumishwa na yanaendelezwa pamoja na kuuendeleza na kuudumisha Muungano wetu. Nitahakikisha kwamba, Serikali nitakayoiunda itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, ili kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na tunaendelea kushirikiana katika masuala yote ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii kwa dhamira ile ile ya waasisi wa Taifa letu; Marehemu Baba wa Taifa; Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume. Ndugu Wananchi, Uchaguzi sasa umekwisha, kazi iliyopo mbele yetu ni kushirikiana kwa pamoja katika kuiletea maendeleo nchi yetu. Kila mmoja wetu, kwa nafasi yake, ana wajibu wa kushiriki katika harakati za maendeleo kwa kufanya kazi ya halali na kutambua kwamba mchango wake ni muhimu katika maendeleo ya nchi yetu. Tukumbuke kauli mbiu ya Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi tu. Serikali nitakayoendelea kuiongoza itasimamia misingi ya haki, uwajibikaji, uwazi na usawa kwa wananchi wote bila ya kumbagua mtu yeyote kutokana na itikadi yake, jinsia au eneo analotoka. Sote ni wamoja na tuna haki ya kunufaika na huduma pamoja na rasilimali zilizopo nchini kwa misingi ya usawa. Ndugu Wananchi, Utendaji wa Serikali na uzoefu nilioupata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ulituwezesha kuitekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu kwa asilimia tisini. Kutokana na mbinu tulizozitumia na uzoefu tulioupata pamoja na kasi na ari tutakayoiongeza, ninaamini kwamba tutafanikiwa kwa asilimia kubwa kuitekeleza 7 Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya 2015/2020. Kwa mnasaba huu, napenda nitoe shukurani kwa viongozi wote nilioshirikiana nao; katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Viongozi hao ni Waheshimiwa Makamo wa Rais, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Watendaji na Watumishi wote wa Serikali katika ngazi mbali mbali kwa kunipa ushirikiano mkubwa. Napenda nikushukuruni kwa utumishi wenu bora katika kuwatumikia wananchi wetu kwa uadilifu, mapenzi na ufanisi mkubwa. Nitaendelea kusimama kidete katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili nchi yetu katika sekta za kiuchumi na ustawi wa jamii. Ndugu Wananchi, Leo si siku ya hotuba ndefu, kwa vile, maelezo ya kina kuhusu mwelekeo wa majukumu na vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika kipindi chake cha pili nitayatoa katika hotuba yangu ya kulizindua Baraza la Tisa la Wawakilishi katika muda mfupi ujao. Ninachoahidi ni kuunda Serikali makini itakayozingatia nidhamu na maadili ya viongozi na watumishi, utendaji kazi wenye viwango bora na maslahi ya nchi yetu katika kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha huduma za jamii kwa kuzitumia vyema rasilimali zetu kwa manufaa ya wananchi wetu. Ndugu Wananchi, Kabla sijamaliza hotuba yangu, nachukua nafasi kuwashukukuru kwa dhati viongozi wote wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania mkiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waheshimiwa Marais wastaafu, Viongozi wa CCM, Waheshimiwa Mawaziri na Viongozi mbali mbali kwa kuja kujumuika nasi katika tukio hili muhimu la kihistoria kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Kadhalika, tunawashukuru sana waheshimiwa Mabalozi na wawakilishi wa mashirika mbali mbali ya Kimataifa ambao wamekuja kushirikiana nasi hivi leo. Kuwepo kwenu ni ithibati ya uhusiano na mashirikiano mema yaliyopo kati ya nchi zetu pamoja na taasisi mnazoziwakilisha. 8 Ndugu Wananchi, Natoa shukurani kwa viongozi wote wa dini waliojuimika nasi leo hii, hapa katika Uwanja huu, kwa ajili ya kuitakia kheri na mafanikio nchi yetu katika Awamu ya Pili ya Serikali nitakayoiunda. Kadhalika, shukurani zangu nazitoa kwenu ndugu wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizi za uapishaji. Naipongeza na kuishukuru Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa, inayoongozwa na Mwenyekiti wake; Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Kamati Maalum ya Sherehe ya Kuapishwa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, inayoongozwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi; Dk. Abudlhamid Yahya Mzee, kwa maandalizi mazuri na kufanikisha sherehe yetu hii ya uapishaji. Hongereni sana. Shukurani zangu, vile vile, nazitoa kwa vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa kuandaa gwaride lililoonesha ukakamavu mkubwa na kuzipamba sherehe hizi. Aidha, natoa shukurani kwa vijana wetu wa halaiki na vikundi vya sanaa vilivyotuburudisha katika siku hii ya leo. Natoa shukurani maalum kwa wageni wetu waalikwa wote waliokuja kushirikiana nasi katika sherehe hizi. Tumuombe Mwenyezi Mungu, azidi kuijaalia nchi yetu amani, umoja na masikilizano. Mwenyezi Mungu atuwezeshe kuyatekeleza yote tuliyojipangia kwa manufaa ya nchi yetu na wananchi wake. Nakutakieni nyote kila la kheri na mrudi nyumbani salama. MUNGU IBARIKI ZANZIBAR MUNGU IBARIKI TANZANIA MUNGU IBARIKI AFRIKA MAPINDUZI DAIMA Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Official Reports
MUONGOZO WA KUOMBA KIBALI CHA UTAFITI-Date Posted: 17-09-2018
FOURTH SCHEDULE (KIAMBATANISHO)-Date Posted: 17-09-2018
RESEARCH/FILMING APPLICATION FORM -Date Posted: 17-09-2018
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO MHE. DKT. KHALID SALUM MOHAMED KUHUSU MAPENDEKEZO YA BAJETI YA SERIKALI (MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI) KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018 -Date Posted: 25-07-2018
RATIBA YA MKUTANO WA KUMI WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI UTAKAOJADILI BAJETI YA SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019-Date Posted: 10-05-2018

Research

Procedure
Research in Zanzibar
Publications
Conferences
PROJECTS

Ongoing Projects
Upcomming Projects
Previous Projects
Reports in Projects
Publication from Projects
GALLERY

Government Activies
Kilimo